Showing posts with label Kimataita - Kenya. Show all posts
Showing posts with label Kimataita - Kenya. Show all posts

Tuesday, April 29, 2014

Sketi fupi a.k.a kimini chamtia mashakani polisi Kenya


http://wscdn.bbc.co.uk/worldservice/assets/images/2014/04/29/140429082123_police_akirt_512x288_bbc_nocredit.jpg
Afisa mmoja wa polisi mwanamke nchini Kenya amepewa onyo kali kwa kuvalia sketi iliyokuwa imembana kiasi cha kuonyesha umbo lake.Wakuu wake walichukua hatua ya kumuonya polisi huyo baada ya picha yake kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kupigiwa gumzo kubwa.

Alipigwa picha akiwa amevalia sketi yake fupi na yenye kumbana akiwa anashika doria katika eneo ambako mashindano ya magari yalikuwa yanafanyika eneo la Kati mwa Kenya. Afisa huyo kwa jina Linda Okello, alitakiwa kufika mbele ya mkuu wake James Mugeria na kuonywa vikali dhidi ya kuvalia hivyo kwa mara nyingine, kitendo ambacho alifahamishwa kuwa ni utovu wa nidhamu kwa kuvalia nguo isiyo ya heshima kwa polisi

Maafisa mjini Kiambu walisema kuwa kupewa onyo kwa afisa Linda na kuonywa dhidi ya kuvalia sketi yake iliyokuwa imembana sana ni jambo la kawaida na kwamba ameruhusiwa kuendelea na majukumu yake. Waliongeza kuwa afisa huyo ameamrishwa kuanza kuvalia kiheshima.

Alipigwa picha na mwanahabari mmoja wa gazeti moja maarufu nchini Kenya akiwa na wenzake kazini mjini Kiambu. Lakini punde si punde picha hiyo ikaanza kusambazwa kwa mitandano ya kijamii na baadhi wakiikejeli. Taarifa ya polisi huyo kuonywa ilizua hasira kwenye mitandao ya kijamii baadhi wakihoji ikiwa ni makosa kwa afisa wa polisi kuvalia sketi ya kumbana.

Source: BBC Swahili

Friday, April 04, 2014

Mwalimu amuua mwanafunzi Kenya

http://wscdn.bbc.co.uk/worldservice/assets/images/2014/04/03/140403123409_mtoto_akichapwa_304x171_bbc_nocredit.jpg

 Adhabu ya kiboko kwa wanafunzi imeharamishwa katika shule zote nchini Kenya
Wazazi katika kaunti ya Kirinyaga mkoa wa Kati nchini Kenya wameandamana kwa hasira baada ya mwalimu kumchapa mtoto mmoja wa shule ya msingi hadi akafariki.
Mtoto huyo inaarifiwa alichapwa kichwani na mwalimu na kuzirai. Alifariki alipokuwa anapelekwa hospitalini.
 
Wazazi hao waliandamana kwa amani wakitaka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya mwalimu huyo.
Hata hivyo polisi waliweza kumkamata mwalimu huyo na kumpeleka kituoni huku uchunguzi ukianza kufanywa.
Mtoto huyo alikuwa katika darasa la saba katika shule ya kibinafsi ya Roka Preparatory.
Inaarifiwa alizirai baada ya mwalimu kumchapa kwenye kisogo.
 
Wazazi hao waliokuwa wanalalamikia kile wanachosema ni wanafunzi kuadhibiwa vikali kwa makosa madogomadogo walitaka mwalimu huyo achukuliwa hatua kali kwa kitendo hicho cha kumchapa mwanafunzi ambacho kimeharamishwa katika shule zote nchini Kenya.

Wengi wa wazazi wenye watoto wao katika shule hiyo wameahidi kuwahamishia shule nyingine.
 Kenya iliharamisha kitendo cha kuwachapa wanafunzi wa shule karibu miaka kumi iliyopita. Ilikuwa baada ya visa vya walimu kuwaadhibu vikali wanafunzi na kuwajeruhi kukithiri.
 
 Kwa msaada wa BBCSwahili.com