Monday, January 20, 2014

Mabadiliko baraza la mawaziri Tanzania


Rais Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri kwa kuwateua mawaziri na manaibu waziri, kuziba nafasi zilizoachwa na mawaziri wanne waliojiuzulu na mmoja aliyefariki dunia hivi karibuni. Katika uteuzi huo Rais Kikwete amewateua mawaziri wapya wawili na manaibu waziri wapya wanane, huku akiwapandisha vyeo manaibu waziri wanne kuwa mawaziri kamili. Miongoni mwa mawaziri wapya ni pamoja na aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dokta Asha-rose Migiro, ambaye ameteuliwa kuwa waziri wa Katiba na Sheria, huku Dk. Titus Kamani akiteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Waziri pekee aliyeachwa katika mabadiliko hayo ni aliyekuwa waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa. Miongoni mwa manaibu waziri wapya ni pamoja na Juma Nkamia ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari na mtangazaji, ambaye amepewa dhamana katika Wizara ya Habari, Vijana na Michezo.
Mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kikwete yametokana na kujaza nafasi za mawaziri ambao walilazimika kujiuzulu baada ya ripoti ya bunge kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili kubaini kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, utesaji na udhalilishaji vikidaiwa kutendwa na watekelezaji wa operesheni hiyo.

Ripoti hiyo iliwalazimisha waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kutangaza kujiuzulu, huku naye waziri wa mambo ya ndani, Dr. Emmanuel Nchimbi kufuata mkondo huo bila kumwaacha waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, Shamsi Vuai Nahodha, na Dr. Mathayo David Mathayo aliyekuwa waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kutokana na wizara zao kuhusika katika usimamizi wa operesheni hiyo ambayo iliwahusisha polisi, askari jeshi na walizni wa wanyamapori. Huku nafasi ya tano katika baraza hilo ikiachwa wazi na aliyekuwa waziri wa fedha, Dr. William Mgimwa aliyefariki dunia mapema mwezi huu nchini Afrika Kusini alikokuwa akipata matibabu.

No comments:

Post a Comment