Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri kwa kuwateua
mawaziri na manaibu waziri, kuziba nafasi zilizoachwa na mawaziri wanne
waliojiuzulu na mmoja aliyefariki dunia hivi karibuni. Katika
uteuzi huo Rais Kikwete amewateua mawaziri wapya wawili na manaibu waziri wapya
wanane, huku akiwapandisha vyeo manaibu waziri wanne kuwa mawaziri kamili. Miongoni
mwa mawaziri wapya ni pamoja na aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Dokta Asha-rose Migiro, ambaye ameteuliwa kuwa waziri wa Katiba na
Sheria, huku Dk. Titus Kamani akiteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi.
Waziri pekee aliyeachwa katika
mabadiliko hayo ni aliyekuwa waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais,
(Mazingira), Dk. Terezya Huvisa. Miongoni mwa manaibu waziri wapya ni pamoja na
Juma Nkamia ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari na mtangazaji, ambaye
amepewa dhamana katika Wizara ya Habari, Vijana na Michezo.
Mabadiliko yaliyofanywa na Rais
Kikwete yametokana na kujaza nafasi za mawaziri ambao walilazimika kujiuzulu
baada ya ripoti ya bunge kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili kubaini kuwepo
vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, utesaji
na udhalilishaji vikidaiwa kutendwa na watekelezaji wa operesheni hiyo.
Ripoti hiyo iliwalazimisha
waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kutangaza kujiuzulu,
huku naye waziri wa mambo ya ndani, Dr. Emmanuel Nchimbi kufuata mkondo huo
bila kumwaacha waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, Shamsi Vuai Nahodha,
na Dr. Mathayo David Mathayo aliyekuwa waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
kutokana na wizara zao kuhusika katika usimamizi wa operesheni hiyo ambayo
iliwahusisha polisi, askari jeshi na walizni wa wanyamapori. Huku nafasi ya
tano katika baraza hilo ikiachwa wazi na aliyekuwa waziri wa fedha, Dr. William
Mgimwa aliyefariki dunia mapema mwezi huu nchini Afrika Kusini alikokuwa
akipata matibabu.
No comments:
Post a Comment