Mwanamume
mmoja nchini China amenusurika kifo katika hifadhi ya wanyama pori nchini humo,
baada ya kujirusha ndani ya hifadhi hiyo akisema alitaka 'kuwalisha' wanyama
hao hatari.
Mwanamume huyo
alitaka kujitoa uhai kwa kujirusha ndani ya chumba cha kuhifadhia Chui wakubwa
wenye Milia au Tiger katika hifadhi ya wanyamapori nchini China. Wageni
waliopigwa na mshangao, walitizama mwanamume huyo aliyejulikana kama Yang
Jinhai, mwenye umri wa miaka 27 akiumwa, kugwaruswa na kubururwa na wanyama hao
kabla ya walinzi kumuokoa.
Kwa mujibu wa
gazeti la kila siku la China, Chengdu, watalii waliokuwa katika hifadhi hiyo
walidhani kuwa bwana Yang alikuwa mmoja wa wafanyakazi wa hifadhi hiyo kwani
walioshuhudia wanasema walimuona akibeba begi mabegani na kupanda mti kama
aliyetaka kuwalisha wanyama hao wakubwa.
Lakini baada
ya watalii kuanza kumpigia mayowe wakimtaka arejee, bwana Yang alijirusha
kutoka mtini na kuanguka ndani ya sehemu walimokuwa wamefungiwa Chui hao.
Watalii hao
walisema kuwa Yang alijirusha akitaraji kuwa Chui hao wangemshambulia na kumuua
, lakini wanyama hoa waliokuwa Chui Milia Dume na Jike walionekana kushtuka
zaidi kwa kumuona Yang huku Chui jike akitoroka kuliko kutaka kumla Yang.
Bwana Yang
alionekana akijaribu kuwafanyia vitendo vya kuwakasirisha ili wanyama hao
waweze kumshambulia lakini hakufanikiwa. Hatimaye Chui Dume alimshambulia Yang
baada ya kushikwa na hasira na kuanza kumuuma na kumgwara lakini aliokolewa na
walinzi wa hifadhi hiyo.
Yang alipata
matibabu lakini baada ya kutibiwa aliwaambia waandishi wa habari kuwa nia yake
ilikuwa 'kuwalisha wanyama hao. Familia ya Yang ilisema kuwa alikuwa na matatizo
ya kiakili na kuwa walikuwa wamepanga kumpeleka hospitalini kwa ushauri nasaha.
Walinzi wa
hifadhi hiyo walisema kuwa Yang alikuwa na bahati mno kuweza kunusurika kifo.
Kwa msaada wa
BBCSwahili.com